Utapeli Mkubwa Waibuka 40 ya Mzee Majuto

NancyTheDreamtz
AMA KWELI kufa kufaana! Hayo ndiyo maneno unayoweza kusema endapo yatakufikia madai ya utapeli mzito unaofanywa na baadhi ya watu wakiwemo wasanii wa kuchangisha pesa kinyume na taratibu wakidai eti ni kwa ajili ya kufanikisha 40 ya marehemu Amri Athumani ‘Mzee Majuto’ inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Taarifa hiyo ya kushtua ilipenyezwa na mmoja wa wasanii wa komedi Bongo, Jabir Ally ‘Wajajo’ ambaye alidai kuwa, akiwa katika mishemishe zake Mitaa ya Kariakoo jijini Dar alikumbana na baadhi ya wafanyabiashara waliohoji juu ya uhalali wa watu hao kuchangisha michango ya 40 hiyo.

Alisema: “Kuna jambo la kushangaza sana nimekutana nalo huku Kariakoo, kuna watu wanapita kwenye maduka na kuomba michango ya kufanikisha 40 ya Mzee Majuto, mimi sikuwa na taarifa ya utaratibu huo, nikahisi kuna utapeli unafanyika.

“Lakini katika kufuatilia nikagundua yupo pia msanii aliyewahi kufanya kazi kwa karibu na Majuto, Bi Rehema, naye anapita kuomba michango, nilipomuuliza akasema eti amepewa hilo jukumu.

“Nikaamua kumpigia kiongozi wetu, Mzee Sumaku ambaye alisema hana taarifa za michango hiyo, nikampigia na msemaji wa TAFF, naye akasema hajui chochote na kama kuna watu wanafanya hivyo, wanakosea sana.”

WAJAJO ATOA USHAHIDI
Katika kuthibitisha madai hayo, Wajajo alitoa namba za simu za watu wapatao watano aliozungumza nao na kumhakikishia kuwa walitoa michango yao baada ya kufuatwa bila kujua kuwa wanatapeliwa.

MSIKIE MMOJA WAO
Akizungumza na Risasi Jumamosi, dada aliyejitambulisha kwa jina la Zulfa Said ambaye ni mfanyabiashara maeneo ya Msimbazi, Kariakoo alisema kuwa, walimpitia watu wawili kwa nyakati tofauti wakidai wanakusanya michango kwa ajili ya 40 ya Majuto, lakini alitoa kwa mmoja shilingi elfu 20, yule mwingine akamwambia alishachanga.

“Mimi nilikuwa mpenzi mkubwa wa kazi za Majuto, kifo chake kiliniuma sana na ndiyo maana walipokuja hao watu niliwiwa kuchanga, nimeshangaa kusikia kuwa wale watu ni matapeli, yaani nimesikitika sana,” alisema Zulfa.

BI REHEMA ATAFUTWA
Kufuatia madai hayo mazito kuwa miongoni mwa watu waliopita ni muigizaji maarufu anayefahamika kwa jina la Bi Rehema, mwandishi wetu alimtafuta ambapo alipopatikana alisema kuwa, ni kweli alipita kwenye baadhi ya maeneo kuchangisha baada ya kuridhiwa na familia ya Mzee Majuto, lakini aliona mwitikio ni mdogo hivyo akaacha.

“Mimi siyo mchangishaji ila kulikuwa na wadada fulani walisema tuchangishe, nikaanza kupitisha daftari watu wanachanga bukubuku tu kwa hiyo nikapata elfu 15 tu, nikaona bora tu niachane nayo maana hata kwenye uchangishaji wenyewe umeshakuwa mgumu, nilimshirikisha mtoto wake (Majuto) Hamza kuhusiana na hilo la kuchangisha, lakini sasa hivi sifanyi tena,” alisema Bi Rehema.


FAMILIA YA MAJUTO INA TAARIFA?
Kufuatia maelezo ya msanii huyo kuwa mtoto wa Mzee Majuto, Hamza Athumani anazo taarifa za uchangishaji huo, mwandishi wetu alimtafuta ambapo alipopatikana alionesha kushangazwa na uchangishaji huo na kucharuka kuwa, huko ni kuchafuana.

“Jamani kweli kufa kufaana, 40 ya mzee ichangishwe Kariakoo? Ni kitu ambacho hakiwezekani na anayesimamia hilo suala la 40 ya baba ni mjomba na hakuna mtu aliyenitaarifu hilo hata siku moja, huko ni kuchafuana,” alisema Hamza ambaye kwa sasa ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.

Mzee Majuto alifariki dunia Agosti 8, mwaka huu ambapo 40 yake inatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Comments

Popular posts from this blog

UCHAGUZI KENYA: Mchezaji wa zamani wa Inter Milan, McDonald Mariga kutoana jasho na Prezzo

Siri Yafichuka, Prince Dube Anakwenda Yanga Kuziba Nafasi ya Fiston Mayele