NancyTheDreamtz Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwaongoza maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha katika hafla ya uzinduzi wa jengo la kitega uchumi la Jakaya Kikwete Ngorongoro Tower (JKNT). Jengo hilo la ghorofa 16, ambalo ni mali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), linatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Septemba 16, mwaka huu. Akizungumza na waandishi wa habari wakati walipotembelewa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha, kukagua jengo hilo, Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Profesa Abiud Kaswamila, alisema Makamu wa Rais amethibitisha kuhudhuria katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo. Alisema jengo hilo ni kati ya majengo ya kisasa zaidi kujengwa mkoani hapa na litatumika maalum kama kituo kimoja cha kukuza na kurahisisha biashara ya utalii nchini. Maneja wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo, Profesa Camillius Lekule, ambaye ndiye aliyebuni mchoro wa jengo hilo, alisema kiasi cha fedha zilizotumika hadi sasa ni Sh. bilioni 39.9 kati ya Sh. bil...