Makocha 60 Waomba Kumrithi Eymael Yanga SC



JUMLA ya makocha 60 wamewasilisha wasifu ‘CV’ za maombi ya kuifundisha Yanga katika msimu ujao wakimrithi aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael.



Eymael alifutwa kazi ndani ya Yanga, Julai 27, mwaka huu baada ya kueneza taarifa zilizokuwa na viashiria vya ubaguzi wa rangi jambo ambalo linapigwa vita na familia ya michezo duniani kote.



Timu hiyo hivi sasa ipo kwenye mchakato wa kumpata kocha mwingine na tayari wapo wanaotajwa kuifundisha Yanga ambao baadhi yao ni Hans Pluijm (Mbelgiji), Ernie Brandts (Mholanzi), Patrick Aussems (Mbelgiji) na Hitimana Thierry (Mrundi).





Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, bado uongozi wa Yanga unaendelea kupokea CV za maombi mengine ya makocha wakuu na wasaidizi kutoka nje na ndani ya nchi.



Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, wamepanga kufunga zoezi hilo la kupokea CV wiki ijayo na haraka watakutana na kuyapitia majina ya makocha hao kabla ya kufanya maamuzi sahihi ya kumteua kocha sahihi.



Aliongeza kuwa vigezo watakavyoviangalia ni uzoefu wa michuano ya kimataifa Afrika bila ya kuangalia uraia wake na makombe aliyoyachukua akiwa anafundisha.“Ndani ya wiki mbili hizi kocha mkuu mpya wa Yanga atajulikana baada ya kumfukuza Eymael, hivi sasa uongozi unapitia CV za makocha mbalimbali waliotuma maombi ya kuja kufundisha.



“Wakati zoezi la kumpata kocha mkuu likiendelea ambalo litachukua wiki mbili, pia uongozi upo katika hatua za kumpata kocha msaidizi ambaye ndani ya wiki moja atapatikana na kutangazwa.



“Kocha huyo msaidizi ataanza na timu katika maandalizi ya msimu mpya wa ligi kabla ya kocha mkuu kupatikana ambaye yeye zoezi lake litachukua muda mrefu kwa lengo la kumpata kocha atakayefaa,” alisema mtoa taarifa huyo. Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Simon Patrick hivi karibuni alisema kuwa: “Uongozi unaendelea kupokea maombi ya makocha mbalimbali waliowasilisha CV zao za kuomba kuja kufundisha Yanga.“Tutahakikisha tunafanya uamuzi sahihi kwa kuteua kocha atakayetufaa kutokana na ukubwa wa klabu yetu ya Yanga.”



SAID MAULID APEWA MIKOBA

Wakati huohuo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Said Maulid, anatarajia kusimamia zoezi la mchakato wa usajili ndani ya klabu hiyo kwa kutoa ushauri wa tathmini ya msimu uliopita kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao kutokana na timu hiyo kutokuwa na makocha kwa sasa.



Taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata kutoka Yanga zinasema kuwa, SMG anatarajia kuwa msemaji mkuu katika benchi la ufundi la Yanga katika kikao cha Jumatatu cha kutoa tathmini ya kikosi na mchakato wa usajili msimu ujao.


NancyTheDreamtz

Comments

Popular posts from this blog

Mbwana Misosi avurugwa: Unanivimbia wewe nani? mimi staa kabla yako, kama wewe sio shabiki yangu basi demu wako shabiki yangu (Video)