Waziri Mkuu: Serikali Inafanya Mapitio Ya Leseni Za Uchimbaji

NancyTheDreamtz
Waziri Mkuu: Serikali Inafanya Mapitio Ya Leseni Za Uchimbaji
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inafanya mapitio ya leseni zote za uchimbaji wa madini na zile ambazo zitabainika kuwa hazijafanya kazi kwa muda mrefu zitachukuliwa na kisha maeneo hayo hayo yatagawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Amesema Wizara ya madini imeimarishwa  na sasa inatengeneza fursa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu inayopatikana katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Mji Mdogo wa Katoro.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Novemba 30, 2018) wakati akizungumza na wananchi katika Mji Mdogo wa Katoro uliopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Geita, akiwa kwenye siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Geita.
Waziri Mkuu amewaambia wananchi hao ambao wengi wao ni wachimbaji wadogo kuwa waendelee kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuhakikisha wachimbaji hao wanafanya shughuli zao bila ya kubugudhiwa.

“Jipangeni kwa kufanya kazi maeneo yapo na Serikali itawapa. Nawashauri mjiunge katika vikundi vitakavyosajiriwa na kutambilika kisheria ili muende kwenye mabenki mbalimbali na kukopa fedha za kununulia mitambo ya kisasa itakayowawezesha kuchimba kwa kutumia teknolojia ya kisasa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Geita ihakikishe kila kijiji kinakuwa na kisima cha maji ili kuwapunguzia wananchi kutumia muda mwingi kwa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji katika maeneo yasiyojulikana.

Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama inayowakabili wanachi kwenye Mji Mdogo wa Katoro, Waziri Mkuu amewataka waendelee kuwa na subira kwani Serikali imepanga kuwafikishia maji kutoka ziwa Victoria.

Waziri Mkuu amesemaSerikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuimarisha huduma za maji  kwenye Mji Mdogo wa Katoro, pia Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya na kikuwezesha Kituo cha Afya cha Katoro kiweze kuwa na maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, chumba cha kujifungulia, wodi za wanawake na wanaume.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema Serikali imeendelea kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo na wa Mji Mdogo wa Katoro ili waendelee kufanya shughuli zao bila ya usumbufu wa aina yoyote.

Amesema katika kuhakikisha wachimbaji hao wafanya shughuli za uchimbaji kwa weledi, Serikali imeamua kujenga vituo vya mfano vyenye lengo la kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu namba bora ya uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa

Amesema Mji Mdogo wa Katoro ni miongoni mwa maeneo ambayo Serikali imejenga kituo hicho katika eneo la Lwamgasa. Pia amesema wachimbaji wadogo kwa sasa wanaendelea na shughuli zao katika maeneo mbalimbali kwa uhuru na Amani yakiwemo ya Bingwa, Musasa, Nyamalimbe, Nyarugusu, Lwamgasa.

Naibu Waziri huyo ametaja maeneo mengine nchini ambayo Serikali inaendelea na miradi ya ujenzi wa vituo hivyo kuwa ni pamoja na Lindi, Chunya, Mpanda, Tanga na   Buhemba mkoani Mara.

Naye, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewahakikishia wakazi wa Mji mdogo wa Katoro na Buselesele kuwa maeneo yao yote ambayo hajaunganishiwa umeme wasiwe na wasiwasi umeme utawaka kabla ya sikukuu ya X-Mass. Amesema mkandarasi tayari ameshafika kwenye maeneo hayo na kuanza  kazi.

Dkt. Kalemani amesemaSerikali maeneo hayo yatasambaziwa umeme kupitia Mradi wa Nishati Vijijini (REA) na wananchi hawatowajibika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwani tayari gharama hizo zimeshabebwa na Serikali.

“Rais wetu Dkt. John Magufuli anataka kuona nyumba ya kila Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na ametenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh. 27,000 tu.”

Awali, Mbunge wa Busanda, Lolencia Bukwimba alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya kwa kuwa kituo chilichopo hakitoshelezi mahitaji kwani watu wengi. Ameomba Serikali iwajengee hospitali na kuimarisha huduma za mama na mtoto kwa kuwa kwa mwezi wanazaliwa watoto 700.

Comments

Popular posts from this blog

UCHAGUZI KENYA: Mchezaji wa zamani wa Inter Milan, McDonald Mariga kutoana jasho na Prezzo

Siri Yafichuka, Prince Dube Anakwenda Yanga Kuziba Nafasi ya Fiston Mayele