Lowassa Akanusha Madai ya Kutaka Kuhamia CCM...." Sina Huo Mpango, Msinigombanishe na Rais

Lowassa Akanusha Madai ya Kutaka Kuhamia CCM...." Sina Huo Mpango, Msinigombanishe na Rais"
Hatimaye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amejibu mapigo ya taarifa zilizokuwa zimesambaa kuwa anawatanguliza watu CCM ili baadaye  ahamie.

Akizungumza mwishoni  mwa wiki iliyopita katika jimbo la Monduli, Lowassa alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa wanaoeneza taarifa hizo ni waongo na wambea.

Mbunge huyo wa zamani wa Monduli ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani alimjibu aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga akimtaka aweke wazi sababu zilizomfanya ahame  kwakuwa ni haki yake ya kikatiba bila kutumia jina lake kwa uongo.

“Waambieni waache umbea na uongo. Anasema uongo kwa kinywa chake. Mimi nimtangulize kwani mimi sina miguu?” alisema Lowassa huku akisisitiza kuwa hana mpango huo.

“Wanasema eti mimi nimekubaliana na Magufuli kuwahamisha wabunge kwenda CCM. Acheni kunichonganisha na Rais, mimi sina mpango wowote na [Rais] Magufuli,” alisema.

Aliongeza kuwa kinachofanywa na wanaohama ni haki yao na wanapaswa kuwaeleza ukweli wananchi kuwa ni shida zao binafsi. Aidha, alimvaa Kalanga akidai kuwa alikuwa na mikopo ambayo imelipwa na kumfanya ahame.

Lowassa ambaye alikuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20, aliwataka wananchi hao ‘kumtoa tongotongo’ kwenye uchaguzi wa Ubunge wa marudio akiahidi kuwa angerejea hapo kwa ajili ya kufanya kampeni za ubunge.

Aliwataka wananchi wa eneo hilo kupuuzia taarifa kuwa hakuna maendeleo ambayo yanafanyika Monduli akiwataka kukumbuka maendeleo ambayo waliyashuhudia alipokuwa mbunge.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliwahakikishia wana Monduli kuwa bado yuko imara kwenye kambi ya upinzani na kuwataka kutoyumba huku akitolea mfano Nigeria ambako wanasiasa takribani 600 wamehama vyama vyao. Alisema suala la kuhama vyama ni la kawaida kwa wanasiasa  hivyo lisiwashtue bali liwafanye wawe imara zaidi.

Joto la uchaguzi wa Ubunge Monduli limeanza kupanda baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Julius Kalanga kujiuzulu na kujiunga na CCM kisha kuchukua fomu ya kugombea tena.

Chadema ambao watakuwa na kibarua cha kutetea jimbo hilo wako katika hatua za kuwachuja walioomba kugombea akiwemo Freddy ambaye ni mtoto wa Lowassa.

Comments

Popular posts from this blog

Mbwana Misosi avurugwa: Unanivimbia wewe nani? mimi staa kabla yako, kama wewe sio shabiki yangu basi demu wako shabiki yangu (Video)