Dah! Stori ya Kanye West Inauma Sana Aisee!


HAINA ubishi, Rapa bilionea, Kanye West ni miongoni mwa marapa bora kuwahi kutokea duniani. Jamaa ni bonge moja la mwimbaji kutoka pale Atlanta nchini Marekani.

 

Ni prodyuza wa muziki wa Hip Hop. Anashikilia rekodi kibao kwenye mauzo ya muziki wake ambao umeuza nakala nyingi zaidi na kumfanya kupendwa sehemu kubwa ya Sayari ya Dunia, huku akiingiza mkwanja wa kutisha.

 

Anatajwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani bilioni 1.3 (zaidi ya shilingi trilioni 2 za Kitanzania) akiwa nyuma ya Jay-Z. Ripoti za thamani za wanamuziki duniani zinaonesha kuwa, ukimtaka Kanye West kwa ajili ya shoo kwa baadhi ya mabara kama Ulaya na Afrika (ikiwemo Tanzania), siyo chini ya Dola za Kimarekani laki 5 (zaidi ya shilingi bilioni moja za madafu).

 

Kanye West amesikika kwa miongo mitatu sasa kwenye ngoma nyingi. Baadhi ya ngoma za Kanye West zilizoweka rekodi nyingi duniani ni pamoja na Otis, Power, Forever, Fade, Good Life, Jesus is King, Jesus is Born na nyingine kibao.

 

Ndoa yake na supastaa wa Tamthiliya ya Keeping Up With The Kardashians, Kim Kardashian imeifanya ndoa yao kuwa maarufu zaidi duniani ikifuatiwa na ile ya Jay-Z na Beyonce.

 

Ni baba mweusi (mwenye asili ya Afrika) akiwa na watoto wanne. Ni mbunifu anayemiliki brandi ya nguo na viatu vya Yeezy.

Kanye West amekuwa akizungumza na kufanya mambo ya ajabuajabu na kushangaza bila kujali nini kitatokea.

 

Wakati f’lani alimshutumu Rais wa zamani wa Marekani, George W Bush kuwa ni mbaguzi wa rangi katika matangazo ya moja kwa moja na akasema ana nguvu za mnyama aitwaye dragon (vampaya au mnyonya-damu).

Alishangaza na kushtua wengi baada ya kumuaibisha jukwaani mwanamuziki Mzungu, Taylor Swift.

 

Hivi karibuni alitangaza na siyo mara ya kwanza, kwamba ana nia ya kugombea Urais wa Marekani.

Yote haya na mengine mengi, yamemfanya kuwa mtu ambaye watu wanapenda kufuatilia maisha yake.

 

Lakini kubwa zaidi ni hivi karibuni, mkewe Kim alijitokeza hadharani na kusema waziwazi kwamba, Kanye West ana matatizo ya afya ya akili (ni kichaa).

 

Hili ni jambo ambalo wengi hawakulifahamu kuhusu Kanye West. Wapo waliodhani ishu hiyo ilipaswa kubakia kuwa jambo la kifamilia na lisilojulikana, kwani ni jambo ambalo limezua gumzo mno hasa wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa Marekani mwaka huu. Suala hilo sasa linajadiliwa na kuzua tafrani mitandaoni hasa Twitter.

 

Baadhi ya watu wamekuwa wakimkejeli. Tabia zake zimekuwa zikiitwa za mtu asiyeeleweka au mwendawazimu, inauma sana aisee!

Hali ya Kanye West inazidi kuzua hofu kila kukicha kutokana na ukweli kwamba, amekuwa wazi juu ya afya yake ya akili.

 

Na hilo lilithibitika alipokusanya watu barabarani na kusema amefungua kanisa ambapo alikuwa akiwahubiria kwa sauti kubwa bila hata maiki!

Mwaka jana, alisema kuwa ana ugonjwa hatari wa bipolar unaomfanya mtu kuwa na hisia au kufanya mambo kupita kiasi, akijielezea kuwa alikuwa katika hali ya hisia za kufanya mambo kupita kiasi na akaomba watu wamuelewe, lakini watu walipuuza.

 

“Ni tatizo la kiafya ambalo lina unyanyapaa mkubwa na watu wanaruhusiwa kusema chochote na kunibagua.

“Ni kama kuteguka ubongo au kuteguka kifundo cha mguu. Na kama mtu ameteguka kifundo cha mguu, huwezi kumkejeli,” alisema Kanye West.

 

Supastaa huyo wa dunia anasema kuwa, wale wanaoelewa matatizo ya akili au hata tabia ya kulazimisha mambo, wanajua kwamba familia huwa haina la kufanya labda mtu awe hajafikisha umri wa kutambulika kama mtu mzima.

Kim Kardashian anasema, mumewe huyo sasa anakosolewa kwa sababu ni mtu maarufu na matendo yake yanaweza kusababisha maoni na hisia kali.

 

“Ni mtu mzuri, lakini ni mgumu ambaye maneno yake wakati mwingine hayaendani na utashi wake,” anasema Kim Kardashian.

Hali ya Kanye West ni ngumu na isiyoeleweka kutokana na ukweli kwamba amekuwa wazi juu ya afya yake ya akili.

Ujumbe mwingi kutoka kwa wataalam wa afya ya akili ni kwamba, hakuna yeyote, hata wenye taaluma, anayeweza kujaribu kubashiri kile ambacho mtu anakipitia, hata awe maarufu kiasi gani.

 

Tetesi hazina budi kuepukwa, wanasema, siyo tu kwa mtu mzuri machoni pa watu, bali kwa uelewa mpana wa afya ya akili.

“Unapaswa kufikiria juu ya watu wote wengine duniani ambao huwenda wanahangaishwa na tatizo la aina hiyo na kufikiria inachomaanisha kwa wale wanaozungumziwa,” anasema Peter Kinderman, Profesa wa Tiba ya Saikolojia wa Chuo kikuu cha Liverpool, Uingereza.

 

Profesa Kinderman anasema tabia zisizo za kawaida, zinaweza kuchunguzwa, lakini ni muhimu zisihusishwe na matatizo ya afya ya akili.

Kwa mujibu wa Mshauri wa Saikolojia, Dk Carolyne Keenan, mtu maarufu anayetoa uelewa juu ya afya ya akili na kusababisha mjadala, inaweza kuwa na athari chanya.

 

“Hatujui ni nani anasimamia akaunti zake za mitandao ya kijamii. Kwa hiyo tunakipa thamani kile ambacho kinatangazwa kwenye mitandao kwamba ni maneno yake, lakini kusema ukweli hatujui,” anasema.

“Kuzungumzia sana mambo magumu kama anavyofanya Kanye West kwa watu wa kawaida, ni tatizo kwa kweli kwa kila mtu ambaye anapitia tatizo la afya ya akili kwa sababu inatoa picha ndogo ya kile ambacho kinaweza kuwa kinaendelea,” anasema.

 

Watu wanapaswa kujibu kwa udadisi na ukaribu kama wanahisi wanahitaji kumjibu Kanye West kwa anachokisema, kufanya au usiseme lolote kabisa.

Wazo la ukarimu linaweza kuwa ni jambo lisilopendwa katika dunia ambayo mara nyingi huwa ni katili kwa watu maarufu na mitandao ya kijamii, lakini licha ya kutuma ujumbe hasi, kumekuwa na ongezeko la hofu na mjadala mpana wa juu ya hatima ya Kanye West.

 

Baadhi ya wachambuzi, waliona kuna unafiki fulani katika kumhurumia, wakielezea ujumbe wa mzaha waliokabiliana nao waimbaji Azealia Banks na Britney Spears, ambao walikabiliwa na maswali kuhusu afya zao za akili baada ya kudaiwa kumkejeli Kanye West.

 

Wengine wanaelezea hofu yao kuhusu nembo za biashara zinazomtumia Kanye West kama balozi wake.

Mwimbaji Halsey anatoa wito kwa watu kuwa na uelewa huku akikiri mwenyewe kuwa anahangaika na tatizo hilo la afya ya akili la bipolar na kwamba si tatizo la kumkejeli mtu, badala yake ni kumsaidia na kumuombea kwa Mungu.

MAKALA: ATLANTA, MAREKANI

NancyTheDreamtz

Comments

Popular posts from this blog

UCHAGUZI KENYA: Mchezaji wa zamani wa Inter Milan, McDonald Mariga kutoana jasho na Prezzo

Siri Yafichuka, Prince Dube Anakwenda Yanga Kuziba Nafasi ya Fiston Mayele