Tundu Lissu Kudai Stahiki zake Mahakamani

NancyTheDreamtz
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema atalifikisha Mahakama Kuu suala la gharama za matibabu yake ili iweze kutoa tafsiri sahihi baada ya Bunge kushindwa kumlipia.

Lissu aliyasema hayo kupitia andiko lake lililoanza kusambaa jana akiwa anatimiza mwaka mmoja tangu alipopigwa risasi Septemba 7, mwaka jana eneo la nyumbani kwake jijini Dodoma.

Katika andiko  lake hilo ambalo pia  ameelezea tukio zima la kujeruhiwa kwake,  mwenendo wa matibabu katika kipindi chote cha mwaka mmoja na kile alichodai kiini cha kuumizwa kwake, kuhusu suala la matibabu ambalo amelifafanua kwa kina  Lissu ametoa sababu za kimazingira na kisheria  ambazo ndio msingi wa yeye kuamua kulifikisha suala hilo mahakamani.

“Kwa upande wetu, njia pekee iliyobaki sasa ni kulipeleka suala hili mahakamani ili Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi ya jambo hili. Maandalizi ya kwenda mahakamani yanaendelea,” alisema Lissu.

Akirejea mvutano kuhusu Bunge kukataa kulipia gharama za matibabu yake,  Lissu aliuelezea kama ‘mgogoro wa kutengenezwa’ ambao katikati yake yumo Spika wa Bunge, Job Ndugai na Katibu wa chombo hicho, Steven Kagaigai ambao wamekuwa wakidai alikiuka taratibu za matibabu ya wabunge kwa kupelekwa Nairobi badala ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwanza.

Katika hilo Lissu alisema utaratibu huo hautambuliki kisheria jambo linaloonekana Spika Ndugai amekubali kuingiliwa na kupokwa madaraka ya Bunge kuendesha shughuli zake kama mhimili huru wa dola.

Akifafanua kuhusu sheria hiyo inayohusika na matibabu ya Wabunge alisema ni Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka  2008 ambayo inaeleza kwa kifupi kwamba kila mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa gharama ya Bunge.

“Utaratibu wa kupata kibali cha Muhimbili, au cha Katibu Mkuu Afya, au cha Rais haupo kwenye Sheria hiyo.

Lissu alisema kama utaratibu huo ungekuwepo kisheria, bado ulikuwa haukidhi na usingeweza kukidhi mahitaji ya dharura iliyotokana na kushambuliwa kwake.

“Kwa majeraha niliyokuwa nayo na kwa hali ya kiusalama iliyokuwepo, hakukuwa na uhakika kwamba nikipelekwa Muhimbili nitakuwa salama dhidi ya watu walionishambulia.

“Na hakukuwa na muda mrefu wa kusubiri hali itulie ndio taratibu zinazosemwa zifuatwe. Ilibidi uamuzi ufanywe haraka ili nikapatiwe matibabu katika hali ya dharura ya kiafya na kiusalama iliyokuwepo”, linasomeka andiko lake hilo.

Alisema uamuzi na taratibu zote za kumpeleka hospitali ya Nairobi haukufanywa na uongozi wa juu wa Chadema peke yao bali ulihusisha viongozi wengine wa Bunge na Serikali  na hivyo kuhoji utaratibu aliokiukwa.

Alisema baada ya kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kilifanyika kikao kilichowahusisha viongozi wa Chadema, Bunge na Serikali kuhusu hatua za kuchukua.

Alisema upande wa Chadema uliongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, na  Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wabunge kadhaa na upande wa Bunge uliongozwa na  Spika Ndugai, Naibu Spika Tulia Akson na Katibu wa Bunge wakati huo, Dk. Thomas Kashililah wakati upande wa serikali alikuwepo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake Dk. Ulisubisya Mpoki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

“Kikao hicho ndicho kilichoamua nipelekwe Nairobi. Ndio maana katika msafara ulionipeleka Nairobi Hospitali, alikuwepo pia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma”, alieleza Lissu.

Kutokana na hayo alisema ndio maana ndege iliyompeleka Nairobi iliruhusiwa kuruka Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa sita usiku.

“Ningekuwa nimepelekwa Nairobi kwa utaratibu binafsi, kama inavyodaiwa sasa, nisingesindikizwa na Mganga Mkuu wa Mkoa na wala Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) isingeruhusu ndege kuondoka Dodoma saa sita usiku.

“Na wala maafisa wa uhamiaji wasingegonga muhuri passport zetu na kuturuhusu kutoka nje ya nchi”, alieleza.

Alisema baada ya kuwa ameshapokelewa hospitali ya Nairobi na maisha yake  kuokolewa, Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kashililah walikutana na ndugu zake kwenye Ofisi ya Bunge Dar es salaam  na kuwashauri waandike barua rasmi ya maombi ili Bunge liweze kutoa fedha za matibabu yangu.

Lissu alieleza kuwa Waziri wa Afya, Ummy naye alishauri hivyo hivyo, tena hadharani kwenye mkutano na wandishi habari.

Alieleza kuwa Ummy alisisitiza jambo hilo kwa kutoa mfano wa Spika wa zamani wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, ambaye inasemekana aliomba msaada wa kutibiwa na Bunge wakati hakuwa Mbunge tena, na tayari alikuwa hospitalini London, Uingereza.

“Barua zikaandikwa na ndugu zangu kama walivyoelekezwa na uongozi wa Bunge. Lakini mara Katibu wa Bunge Kashililah akaondolewa madarakani na Rais Magufuli, na Steven Kagaigai akateuliwa kushika nafasi hiyo”, alieleza.

Alieleza kuwa inavyoonekana Kagaigai alikwenda na maelekezo ya yeye kutopewa fedha yoyote ya matibabu na Bunge.

Comments

Popular posts from this blog

Mbwana Misosi avurugwa: Unanivimbia wewe nani? mimi staa kabla yako, kama wewe sio shabiki yangu basi demu wako shabiki yangu (Video)