Waziri Lugola Awaondoa Madarakani Maafisa Wa NIDA Mkoa Wa Ruvuma
NancyTheDreamtz
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola amemuondoa madarakani Afisa wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoa wa Ruvuma, Seif Mgonja kwa
kosa la kutogawa kwa wananchi Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN),
14,493 tangu Disemba 31, 2019, licha ya kuzalishwa na Makao Makuu na
kuletewa ofisini kwake Mjini Songea.
Pia
Waziri Lugola amemuondoa madarakani Afisa wa NIDA Wilaya ya Namtumbo,
Mkoani humo, Thobias Nangalaba kwa uzembe wa kutofika katika kikao chake
cha viongozi wa Mkoa na Wilaya, licha ya kupewa taarifa ya kuhudhuria
kikao hicho.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Soko Kuu la Manispaa
ya Songea Mkoani humo, leo, Waziri Lugola amesema, amewatengua vyeo
maafisa wawili hao kwa kucheza na kazi za Serikali, kwa kutojali majukumu yao.
“Ndugu
wananchi wa Songea, maafisa hawa wamekuwa wakienda kinyume na maagizo
ya Serikali la kuwataka waweze kuwakamilishia wananchi usajili wa laini
za simu kwa alama za vidole kwa wakati, hivyo hawatufai na wanapaswa
watupishe ili wengine waweze kuiongoza NIDA Mkoani hapa, haiwezekani
Afisa wa NIDA Mkoa anacheza na wananchi kwa kutopeleka taarifa ili
waweze kupata fursa ya kusajili laini zao ambapo zoezi hilo linatarajia
kukamilika Januari 20 mwaka huu,” alisema Lugola.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli
inawajali wanyonge hivyo yeye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ndani ya
Nchi, anapambana na watu wanaokwamisha jitihada za Serikali.
Aidha,
Waziri Lugola aliitaka Idara ya Uhamiaji Mkoani humo kufanya kazi usiku
na mchana wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuwasaka wahamiaji haramu
hasa katika eneo la mpaka wa Tanzania na Msumbiji Mkoani humo.
“Ndugu
wananchi, toeni taarifa za wahamiaji haramu, itasaidia kuwakamata na
pia kuwashughulikia ipasavyo kwakuwa watu hao ni hatari kwa uhalifu,”
alisema Lugola.
Aliongeza
kuwa, Jeshi la Polisi lipo imara na linaendelea kulinda usalama wan
chi, matukio ya uhalifu makubwa yamesambaratishwa, na matukio yaliyobaki
ni madogo
ambayo hayana nguvu katika amani ya nchi.
“Serikali
ya Dkt. John Pombe Magufuli ipo imara, uhalifu sasa haupo, ujambazi
tumeusambaratisha kabisa, kama kuna uhalifu basi mdogo mdogo tu, huyu
kanitukana hivi na vile lakini matukio ya uhalifu makubwa hayapo nchini,
nyie mashahidi na mnaona,” alisema Lugola.
Waziri Lugola anaendelea na ziara yake baada ya kumaliza Mkoa wa Ruvuma, anatarajia kwenda Mtwara na Mkoa wa Lindi.
Comments