Kidato Cha NNE Kuanza Mitihani Leo....Serikali Yatoa Onyo Kwa Watakaoiba Mitihani
NancyTheDreamtz
Mtihani wa taifa wa kidato cha nne unaanza leo, huku Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) likitoa onyo kali kwa watakaobainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu.
Baraza hilo limesisitiza kuwa halitasita kukifutia matokeo kituo chochote cha mtihani ambacho kitabainika kujihusisha na udanganyifu.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mtihani huo ambao utawahusisha jumla ya watahiniwa 427,181.
Dk. Msonde alisema baraza linazitaka kamati za mitihani za mkoa, halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya taifa zinazingatiwa ipasavyo.
“Kamati zihakikishe kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,” alisema.
Alisema wasimamizi wote wanatakiwa kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Wasimamizi wanaaswa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya taifa.
Dk. Msonde alisema kwa upande wa wanafunzi, baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi cha miaka minne ya elimu ya sekondari.
“Matarajio ya Baraza la Mtihani ni kuwa wanafunzi watafanya mitihani yao kwa kuzingatia kanuni za mitihani. Watahiniwa wote watambue kuwa kukiuka kanuni za mitihani au kufanya udanganyifu kutawafanya wafutiwe matokeo yao yote,” alisema.
Alisema baraza linawataka wamiliki wa shule wote kutambua kuwa shule zao ni vituo maalum vya mitihani, hivyo hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyaji wa mtihani huo.
Dk. Msonde alisema hawatasita kukifutia matokeo kituo chochote cha mtihani endapo baraza litajiridhisha kuwapo na uhatarishi wa usalama wa mitihani ya taifa.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mitihani ya kidato cha nne inafanyika kwa maarifa, amani na utulivu.
“Wananchi wanaobwa kuheshimu eneo la mitihani na kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote asiyehusika na mitihani anayeingia kwenye maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani. Tukifanya hivyo, tutawawezesha watoto wetu kufanya mtihani kwa amani na utulivu,” alisema.
Dk. Msonde aliwataka wanafunzi, walimu na wananchi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani huo.
Alisema baraza halitasita kuchukua hatua kwa yoyote atakayejihusisha na udanganyifu katika mitihani kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za utumishi wa umma.
Aidha, aliwaomba wadau wote kutoa taarifa katika vyombo husika kila wanapobaini mtu au kikundi cha watu kujihusisha na udanganyifu wa mitihani ya aina yoyote.
Kwa mujibu wa Dk. Msonde, jumla ya watahiniwa 427,181 wamesajiliwa kufanya mtihani huo ambao utamalizika Novemba 23, mwaka huu.
Alisema kati ya watahiniwa wa shule ni 368,227 na watahiniwa wa kujitegemea ni 58,954.
“Kati ya watahiniwa wa shule 368,227 waliosajiliwa, wanaume ni 180,908 sawa na asilimia 49.13 na wanawake ni 187,319 sawa na asilimia 50.87. Watahiniwa wenye mahitaji maalum wapo 562 kati yao 372 ni wenye uoni hafifu, 44 wasioona, 109 wenye ulemavu wa kusikia na 37 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,” alisema.
Comments