Waziri Jafo Afunguka Sakata la Mkurugenzi Aliyekamatwa Akitaka Kutoroka Nchi Kuelekea Nchi Jirani

NancyTheDreamtz
Waziri Jafo Afunguka Sakata la Mkurugenzi Aliyekamatwa Akitaka Kutoroka Nchi Kuelekea Nchi Jirani
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amesema walimkamata aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’wale, Geita, Carlos Gwamagobe, akitaka kutoroka kwenda nchi jirani baada ya upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 2.2.

Kauli hiyo aliitoa jijini hapa jana wakati akifunga mafunzo kwa wakuu wa wilaya wapya 27 na wakurugenzi 39 walioteuliwa Julai na Agosti, mwaka huu na Rais Dk. John Magufuli.

“Kwa mfano juzi juzi pale Nyang’wale watu wameiba zaidi ya shilingi bilioni 2.2, sio fedha za mchezo eti mfano Halmashauri ya Kakonko inakusanya shilingi milioni 343,” alisema na kuongeza:

“Halmashauri nyingine wameiba shilingi bilioni 2.2 sawa na miaka saba ya ukusanyaji wa Kakonko, lakini muda mfupi watu wamechukua akaunti inasoma ziro.

“Halafu hawana shaka wanafunga mikanda, nimpongeze mkurugenzi wa Nyang’wale, alionyesha ndani ya muda mfupi anafaa kuwa mkurugenzi.

“Alikataa baada ya kuona vitu havijakaa sawa, angeenda kichwa kichwa angewekewa mahindi katika gunia bovu na lingekuja kumpasukia yeye mbele ya safari.

“Yule mkurugenzi tuliyemwona hatoshi tulimtoa tena kwa bahati mbaya alikuwa anakimbia anaenda nchi jirani, amekamatwa akiwa anakimbia na hadi sasa bado tuna watu wa aina hiyo.

“Ndiyo maana tulielekeza wote weka ndani, tumewatia ndani wote na tumetoa maelekezo kwa vyombo vinavyohusika  vifanye kazi kwa mujibu wa sheria.

“Maana kuna staili mtu anasema mimi nafungwa ila watu wangu si wanakula tu. Nimevipa maelekezo kule vyombo vifanye kazi ikibainika kama wana rasilimali zozote ziendelee kushikiliwa na sheria ikiruhusu mali zile zitaifishwe zirejeshwe serikalini, hii ni nchi nyingine tofauti.”

Pia alisema Serikali itaendelea kulinda rasilimali fedha huku akiwataka na wakuu hao wa wilaya na wakurugenzi na wao kuzilinda kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, alisema moja ya sababu zilizofanya wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kutumbuliwa ni kutokana na kukosa nidhamu.

“Naomba niwaambie wenzenu waliotoka, wengine wametoka kwa kigezo cha nidhamu. Jambo lingine ambalo tumejifunza hapa kwa siku zaidi ya tano ni nidhamu, ajenda ya nidhamu ni muhimu kwa mtumishi wa Serikali, wewe mwenyewe kwanza ulivyo, unavyoongea unatakiwa uwe na nidhamu.

“Imani yangu ajenda ya nidhamu itaenda kufanyiwa kazi, niwasihi katika maisha yangu napenda watu wa chini wakue na nina historia hiyo washike nafasi za juu,” alisema.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Musa Iyombe, kuwavua madaraka watendaji wasiotimiza wajibu wao.

“Katibu Mkuu unapoona kuna watendaji mizigo hakuna kuwahamisha ni kuwavua vyeo hakuna namna na nimshukuru sana amefanya kazi hiyo, amepitisha fagio lakini bado wapo,” alisema.

Aliwataka kujua mipaka yao ya kazi ili kupunguza migogoro inayojitokeza.

“Hapa mgogoro mkubwa ndipo unapotokea, nendeni mkachunge mipaka ya kazi, hapa mmejifunza DC mipaka yake inaishia wapi, mkurugenzi mipaka yake inaishia wapi hivyo naamini tutafuata mipaka ya kazi,” alisema Jafo.

Aliwataka kushughulikia kero za wananchi kabla ya viongozi wakubwa hawajafika katika maeneo yao.

“Ninachotaka kila mmoja atimize wajibu wake, leo kiongozi anafika anakuta mabango, kero hazishughulikiwi, hiyo ni kwamba kero hasizikilizwi,” alisema Jafo.

Pia aliwataka kusimamia haki za watu wa chini wanaodhulumiwa na matajiri.

“Kama kuna rasilimali zinatolewa kwa wanyonge na matajiri wamezichukua hili kaliangalieni ili wanyonge warudishiwe, mtu anawanyanyasa watu kwa fedha,” alisema Jafo.

Awali, Iyombe alisema hakuna jambo linalomsikitisha kama wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watendaji.

“Wakuu wa wilaya mnatumia vibaya madaraka yenu hili si jambo linalokubalika, tuzingatie kutumia madaraka yenu ambayo Rais amewaamini.

“Hata ukisema leo, kesho ndiyo wanawasha moto kabisa, unamwona tu huyu hatadumu kabisa, hawa ndio viongozi wetu vijana, wazee tunang’atuka tutawaacha nyinyi.

“Halafu baada ya hapo mbona hujapanda cheo, tumeshuhudia baadhi yenu nimewaandikia ujumbe kwenye simu kwamba unachokifanya si mwongozo wa Serikali, nawaomba zingatieni sheria, kanuni na taratibu na mzisome,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog

Mbwana Misosi avurugwa: Unanivimbia wewe nani? mimi staa kabla yako, kama wewe sio shabiki yangu basi demu wako shabiki yangu (Video)