Hospitali Teule ya Wilaya ya Missenye ya Mugana mkoani Kagera imefanya upasuaji na kutoa kijiko, betri ndogo ya redio na vitambaa kwenye tumbo la mgonjwa wa akili. Vitu vingine vilivyotolewa vilivyokuwa vimeziba njia ya haja kubwa na kumfanya apate maumivu makali ya tumbo ni vibiriti viwili vya gesi, mswaki na ganda la limao. Dk Eliud Nyonyi aliyeshiriki kumfanyia upasuaji mgonjwa huyo amesema baada ya vitu hivyo kutolewa hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri. “Hiyo picha inayosambaa mitandaoni sijaiona, lakini ni kweli kuna mgonjwa tumemfanyia upasuaji na tumemkuta hivyo vitu tumboni, ila siwezi kuzungumzia zaidi taarifa za mgonjwa,” alisema. Picha inayoonyesha vitu hivyo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao mbalimbali huku kila mtu akisema lake kuhusu vitu hivyo. Dk Nyonyi ambaye anakaimu nafasi ya mganga mkuu wa hospitali hiyo alimtaja mgonjwa huyo kuwa ni Eliud Novart (25) na kwamba, bado amelazwa katika wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji akiendelea kupatiwa matibabu. Mganga mkuu...