Ndalichako Ataja Sababu za Wanafunzi Kukacha Hesabu

NancyTheDreamtz

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo asilimia 80 ya wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne, wamekuwa wakifeli somo la hesabu kutokana na sababu mbalimbali.

Ametaja moja ya sababu kuwa ni walimu kutokuwa na mbinu za kuwavutia wanafunzi kupenda somo hilo na kuwavunja moyo pale wanapokosea.

Ndalichako aliyasema hayo juzi wakati akifungua mkutano wa walimu wa masomo ya hesabu kutoka nchi 15 za Afrika, Marekani na Uingereza, ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha Aga Khan kwa lengo la kujadili mbinu za kufundisha somo hilo.

Profesa Ndalichako alisema sababu za wanafunzi kufeli somo hilo ni kutokana na walimu kutokuwa wabunifu wa mbinu mbalimbali za kuwafundishia hali inayosababisha kulichukia.

Alisema kutokana na wanafunzi wengi kufeli, kumekuwa na uhaba mkubwa wa walimu wa somo hilo na kusema kuwapo kwa mkutano huo kutasaidia kuongeza ari kwa walimu kuwafanya wanafunzi walipende.

“Ni asilimia 20 tu ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya kidato cha nne wanafaulu hesabu. Kwa miaka 10 mfululizo takwimu zinaonyesha asilimia 80 ya wanafunzi wote nchini wanafeli hesabu ndiyo maana leo (juzi) hii nimevutiwa kuja kufungua mkutano huu ili niwashawishi walimu kubuni mbinu mbalimbali za kuwavutia wanafunzi kupenda hesabu," alisema Profesa Ndalichako.

Alisema tabia ya walimu wa somo hilo kuwapa wanafunzi alama kubwa ya kosa kuanzia juu hadi chini inasababisha pia wanafunzi wachukie somo hilo na kulikwepa.

“Mwalimu unapompa mwanafunzi kosa kuanzia juu hadi nchini ya karatasi utambue unamvunja moyo na kujiona hawezi kitu ni bora mwanafunzi akaeleweshwa kwa kupewa mrejesho na kuelekezwa njia rahisi zitakazomfanya apende somo hili na mwisho wa siku tuongeze idadi ya walimu wa hesabu," alisema Profesa Ndalichako.

Pia aliwataka walimu hao kujadili tatizo hilo linalozikabili nchi nyingi duniani kwa kuangalia ni kwa namna gani wataondoa dhana iliyojengeka kwa wanafunzi kuwa hesabu ni somo gumu pamoja na kiwashawishi kulipenda.

Naye Mkuu Chuo hicho, Profesa Joe Lugalla, alisema sababu ya Aga Khan kudhamini mkutano huo wa tano kufanyika katika nchi mbalimbali Afrika ni kutokana na mpango wao wa kuboresha sekta ya elimu nchini.

Alisema kama walimu hawajui njia nzuri za kuvutia wanafunzi kupenda somo la hesabu wanasababisha wanafunzi wasielewe wanapofundishwa na ndio sababu ya wengi kufeli.

“Aga Khan tumekutanisha walimu wa nchi 15 za Afrika na Ulaya na Marekani kwa ajili ya kujadili kwa pamoja namna walimu hawa wanaweza kuvutia wanafunzi kupenda somo la hesabu," alisema Profesa Lugalla.

Naye mwanataaluma wa chuo hicho, Profesa Fredick Mtenzi, alisema mkutano huo unaojadili namna nzuri ya kufundisha hesabu una lengo la kubadili aina ya ufundishaji kwa walimu wa somo hilo ambao wameonekana ni tatizo.

Alisema kaulimbiu katika mkutano huo inasema, “ufundishaji mzuri wa hesabu kwa watu wote” itachochea walimu kufundisha vizuri na kusaidia kuchangia katika sekta zote.

Comments

Popular posts from this blog

Siri Yafichuka, Prince Dube Anakwenda Yanga Kuziba Nafasi ya Fiston Mayele

Top Ten ya Makabila Yaliyotoa Wasomi Wengi Nchini Tanzania

Jacqueline Wolper Atamani Kutoka Kimapenzi na Rais