Kwa Ishu ya King Bae Unajitekenya na Kucheka Mwenyewe!

NancyTheDreamtz
ZARINAH Hassan ‘The Boss Lady’ ni miongoni mwa wanamama maarufu Afrika Mashariki ambaye kwa namna moja au nyingine, umaarufu wake umekua zaidi baada ya kukutana na kuzaa watoto na mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.  Wakati penzi lake na Diamond au Mondi linachipukia, watu wengi hususan Wabongo walikuwa hawamjui kivile. Baada ya kuanza uhusiano na Mondi ndipo watu sasa wakaanza kumfuatilia na kujua shughuli zake licha ya kuwa kwenye uhusiano huo bado kulikuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu kwa mrembo huyo.
Watu walikuwa wakihoji kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii anajinasibu na magari mengi ya kifahari yenye namba zilizosomeka Zari1, Zari2 na mengine kibao, je, yalikuwa ni ya kwake kweli kwa maana ya kumiliki au la?
Achana na hilo, kuna lile suala la shule na maduka anayodaiwa kumiliki nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ bado na vyenyewe vilikuwa ni kitendawili. Hakuna aliyeweza kutegua moja kwa moja kama ni kweli anamiliki au la.
Kama hiyo haitoshi, hata katika umiliki wa nyumba kule Sauz bado watu walikuwa hawaamini kama ni kweli ana nyumba licha ya kuelezwa pia ipo aliyoachiwa na marehemu mumewe Ivan Semwanga. Aina ya maisha yake aliyoyaonesha kwenye mitandao ya kijamii, yaliashiria kwamba ni mtu mwenye nazo.
Viwanja anavyotembelea na mialiko anayoipata ilionesha kwamba ni mtu wa hadhi fulani ya juu katika jamii, lakini bado suala la uhakika wa kwamba ni kweli anamiliki ukwasi anaojionesha nao lilikuwa ni mtihani. Unamuona ni mrembo, unamuona ana magari na kila kitu, lakini kuamini linakuwa jambo gumu kutokana na pengine umbali (sababu anaishi Sauz) au pia ukwasi mkubwa anaotamba nao kutofanana na uhalisia wa miradi inayomuingizia kipato.
Bahati mbaya sana wakati maswali hayo yakiwa angali hayapata majibu ya moja kwa moja, akaachana na mwandani wake, Mondi. Hivyo aina ya maisha yake yakabaki kuwa siri huku tukiendelea kuona ‘mapichapicha’ kwenye mitandao ya kijamii.
Pamoja na mambo mengi aliyoyafanya, suala ambalo watu wameshindwa kumuelewa Zari ni juu ya huyu bwana mpya anayedai amefunga naye ndoa na kumtaja kwa jina la King Bae au Mr M. Anamnadi mitandaoni nusunusu, haweki picha yake ‘full’.
Licha ya kelele kuwa nyingi za watu kutaka kuhoji mwanaume gani huyo hatumuoni sura, kudai kwamba atakuwa ni mume wa mtu ndiyo maana hamuoneshi, lakini wapi, bwana Zari ameamua tu kutomuonesha hadharani.
Katika hali ya kawaida, mtu ambaye mna mahusiano huwezi kumficha hivyo. Historia inaonesha, wanaume wake wote aliowahi kuwa nao huko nyuma aliwaonesha tu hadharani mitandaoni. Huyu wa sasa kasoro gani? Kwa nini umfiche? Unamficha ili iweje? Utamficha mpaka lini?
Ndiyo maana nasema kwenye ishu hii Zari anajitekenya na kucheka mwenyewe maana mwisho wa siku atakuja kuumbuka tu kama hakuna huyo mtu anayeitwa King Bae. Mashabiki wanategemea kwamba, kama angekuwa anataka kumrusha roho Mondi kwa maana ana bwana, basi angemuonesha sura na jeuri ya fedha anayomfanyia.
Sisi tupo, tunaweka rekodi zetu sawa tuone jinsi atakavyolimaliza suala hili na hapa ni mawili; amfunue huyo jamaa tumuone kama kweli au apotezee kwa kukaa kimya na tusubirie kumuona shemeji yetu mpya.

Comments

Popular posts from this blog

UCHAGUZI KENYA: Mchezaji wa zamani wa Inter Milan, McDonald Mariga kutoana jasho na Prezzo

Siri Yafichuka, Prince Dube Anakwenda Yanga Kuziba Nafasi ya Fiston Mayele